Kiungo mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi amefunguka kuwa amejipanga kuonyesha kiwango cha hali ya juu kwenye mchezo wa leo ili kuwathibitishia mashabiki ambao wana hofu na uwezo wake baada ya kushindwa kutamba alipokwenda nchini Denmark kabla ya kurudi kwao Uganda.
Okwi aliyetua Simba akitokea SC Villa, ataungana na mastaa wengine wa Simba waliosajiliwa hivi karibuni kuonekana kwa mara ya kwanza wakikichezea kikosi hicho kwenye mchezo wa Simba Day mbele ya Wanyarwanda, Rayon Sports.
Mshambuliaji huyo amesema atabadilisha mawazo ya mashabiki wengi leo ambao walimuona hana jipya baada ya kushindwa kutamba alipokwenda Denmark kwa kuonyesha kiwango cha hali ya juu dhidi ya Rayon Sports.
“Najua mashabiki wengi wana hofu na uwezo wangu kwa sababu muda mrefu umepita baada ya kuondoka hapa Tanzania, lakini niwaambie kwamba kama wanataka kuona nini ambacho nitakifanya basi waje uwanjani katika Simba Day.
“Kile ambacho nitakifanya kwa kila mmoja kitabaki historia, na nikwambie niko vizuri sana na naelewana na wenzangu vizuri baada ya kukaa nao kule Afrika Kusini tulipokuwa kambi,” alisema Okwi.
0 comments:
POST A COMMENT