Leo Alhamisi August 3, 2017 klabu ya Singida United imesaini mkataba wa mwaka mmoja na kampuni ya utengenezaji wa mbolea ya YARA Tanzania kutoka Norway.
Mkataba huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 250 umesainiwa na Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga na Mkurugenzi wa kampuni ya YARA Alexander Macedo.
Mkurugenzi wa kampuni ya YARA, Alexander Macedo amesema wameamua kuidhamini klabu hiyo kwakua anapenda mpira na kilimo na anaamini kupitia wao vijana wengi wa Tanzania watapata ajira.
“Binafsi napenda sana soka na kilimo kwahiyo moja ya sababu iliyonivutia kudhamini klabu hii ni hiyo, nadhani itazalisha ajira kwa vijana wengi wa Tanzania,” – Macedo.
Mkuugenzi wa Singida United Festo Sanga amesema wanaendelea kutafuta wadhamini wengine ambapo kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na makampuni mengine zaidi.
“Singida United ni kampuni kwahiyo tunajishughulisha na mambo mengi ikiwemo kilimo kwahiyo tunaamini udhamini huu utasaidia ekari zetu 10,000 kupata mbolea,” alisema Sanga.
Mbali na kampuni hiyo tayari timu hiyo imeingia mkataba na ya SportPesa, Oryx na Puma kama wadhamini rasmi wa klabu.
0 comments:
POST A COMMENT