Tayari Simba imerejea jijini Dar es Salaam kumalizia maandalizi ya mwisho kabla ya mechi yake ya tamasha la Simba Day ikiivaa Rayon Sports, timu bora kutoka Rwanda kwa kipindi hiki.
Tamasha hilo linafanyika Jumanne na kazi itakuwa ngumu kwa Simba kwa kuwa Rayon wako vizuri na mashabiki wa Msimbazi wangependa kupata ushindi wa kwanza wa Dar es Salaam wakiwa na wachezaji wapya.
Hata hivyo, kipa wa Simba, Aishi Manula anataka kutumia vizuri kila nafasi atakayoipata kukaa langoni kwani anamuhofia Said Mohamed ‘Nduda’.
Wote wawili Manula na Nduda wamejiunga na Simba hivi karibuni ambapo Manula ametokea Azam FC na Nduda akitokea Mtibwa Sugar, wote tayari wapo kambini Afrika Kusini.
Manula alisema Nduda siyo kipa wa kumbeza kutokana na kiwango chake alichonacho hivi sasa akiwa langoni ndiyo maana wote wapo Taifa Stars.
Alisema anafurahia changamoto atakayokutana nayo ndani ya Simba akiwa na Nduda na kipa mwingine Emmanuel Mseje aliyesajiliwa kutoka Mbao FC.
“Nina kibarua kigumu cha kuhakikisha ninapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na hiyo inatokana na kiwango kikubwa alichonacho mwenzangu (Nduda).
“Ninahitaji kucheza kwa kujituma na kutumia vizuri kila nafasi nitakayoipata kudaka nikiwa katika kikosi cha kwanza.
“Lakini tumuachie Kocha Omog (Joseph) kwani ndiye atakayeamua kipa gani mzuri atakayekuwa anapata nafasi ya kucheza,” alisema Manula.
0 comments:
POST A COMMENT