Afisa habari wa Simba Haji Manara ametoa ufafanuzi kuhusu tetesi kwamba beki wao wa kati raia wa Uganda Jjuuko Murushid kujiunga na klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Manara amesema, Jjuuko bado ana mkataba na klabu ya Simba lakini kama kuna timu inahitaji huduma ya mganda huyo wanaikaribisha kwa mazungumzo.
“Juuko bado ni mchezaji wa Simba ana mkatab, tunazungumza nae hivi sasa kuona namna ya kuboresha mkataba wake kwa maana ya kuuongezea lakini kama kuna klabu yoyote ile iwe Orlando Pirates au yoyote inayomtaka basi mazungumzo hayo yanaruhusiwa kufanyika. Simba haiwezi kumzuia mchezaji kwenda kufanya majaribio kwa hiyo Juuko atakuja muda wowote kuungana na wenzake.”
“Suala la kwenda Orlando bado sisi hatuna taarifa rasmi ingawa linaweza likatokea na likitokea kama nilivyosema awali hatutalipinga.”
Julai 25, 2017 mtandao unaoandika habari za michezo nchini Uganda Kawowo Sports waliripoti kwamba, Orlando wameonesha kuvutiwa na beki huyo wa kati ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Uganda kilichocheza fainali za michuano ya Afrika AFCON 2017.
Ripoti zinadai kwamba, Jjuuko alitarajiwa kusafiri tangu juma lililopita kwenda Afrika Kusini lakini alikwama kutokana na kuchelewa kwa visa.
Bado hakuna uhakika kwamba anakwenda kwa ajili ya majaribio au atasaini moja kwa moja mktaba kuitumikia klabu hiyo ambayo ilimaliza katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi kuu ya Afrika Kusini ikiwa na pointi 33 huku ikiwa imefungwa magoli 40 yenyewe ikiwa imefunga mabao 29 pekee.
0 comments:
POST A COMMENT