BARAZA la wadhamini la klabu ya Simba limeendelea kumwekea ngumu mfanyabiasha Mohammed Dewji ‘Mo’ katika suala lake la kutaka kuwekeza hisa za asilimia 51 zenye thamani ya shilingi bilioni 20.
Suala hilo limesababisha mpasuko mkubwa ndani ya klabu hiyo kwani kuna baadhi ya wanachama wanaunga mkono mabadiliko ya uwekezaji wa Mo huku wengine wakipinga wakiongozwa na baraza la wadhamini.
Katibu mkuu wa baraza hilo Mzee Hamis Kilomoni amewaambia Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu hiyo kuwa suala la Wekundu hao kumilikiwa na mtu mmoja halitatokea kamwe.
“Simba imefanya mabadiliko mengi mpaka sasa, tulikuwa hatuna majengo sasa tunayo, tulikuwa hatuna uwanja sasa tunao na ujenzi utaanza hivi karibuni kwahiyo hao wanaotaka mabadiliko wanataka yapi,” alihoji Mzee Kilomoni.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya uongozi wa klabu hiyo kuitisha mkutano mkuu utakaofanyika Agosti 13 ambao moja ya ajenda zake itakuwa mabadiliko ya katiba ili kumwezesha Mo kuwekeza klabuni hapo.
Aidha kutokana na viongozi wakuu wa klabu hiyo Rais Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange kushikiliwa na vyombo vya dola, wadhamini hao wanataka mkutano huo usogezwe mbele hadi suala hilo litakapotoa majibu.
0 comments:
POST A COMMENT